Kisangwa Yapata Neema ya Maji: Esther Bulaya Ashiriki Uzinduzi wa Mradi wa Milioni 716 Bunda
Wananchi wa Kata ya Mchalo, tawi la Kisangwa, Wilaya ya Bunda wamepata tumaini jipya baada ya kuzinduliwa rasmi kwa jiwe la msingi la mradi wa maji unaolenga kuondoa changamoto ya uhaba wa huduma hiyo muhimu.
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, leo Machi 17, 2026 alishiriki katika uzinduzi huo uliokwenda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Maji, tukio lililokusanya viongozi wa kisiasa, wataalamu wa sekta ya maji pamoja na wananc
hi wa eneo hilo.
Uzinduzi huo uliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, huku ukihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWASA), Esther Enock Gilyoma, pamoja na viongozi mbalimbali wa idara ya maji.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bulaya alieleza kuwa mradi huo wenye thamani ya shilingi milioni 716 ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma safi na salama ya maji, huku akisisitiza kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wakazi wa Kisangwa.
Aidha, alimpongeza Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya maendeleo, hususan sekta ya maji, ambayo ina mchango mkubwa katika ustawi wa jamii. Kauli mbiu ya mradi huo ni “Maji na Jinsia”, ikilenga kuonyesha umuhimu wa upatikanaji wa maji kwa usawa.
“Mradi huu unaendana moja kwa moja na dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, kwani wanufaika wakubwa ni kina mama. Niliahidi kushirikiana na viongozi wenzangu kutatua changamoto hii, na leo tumekusanyika hapa kama mashahidi wa utekelezaji wake,” alisema Bulaya.
Kwa upande wao, wananchi wa Kisangwa wameeleza furaha yao juu ya mradi huo, wakiamini kuwa utarahisisha shughuli za kila siku na kuongeza kasi ya maendeleo katika eneo lao.
Mmoja wa wananchi hao, Diana Mgaya, alisema:
“Tunamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, Wizara ya Maji na Mbunge wetu Esther Bulaya kwa kutuletea mradi huu. Huu ni mwanzo wa maendeleo makubwa kwetu.”
Mradi huu unatarajiwa kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii na kiuchumi kwa wakazi wa Kisangwa, huku ukiweka msingi imara wa upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wote



Comments
Post a Comment