MKUU WA WILAYA YA TARIME AKABIDHI MIZINGA KWA WAZEE WA KOO 12 WAZEE WAMSHUKURU NA KUTOA PONGEZI KWA SOYA ONE NA WADAU WENGINE
Tarime, Julai 28, 2025
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, ameendesha tukio maalum la kukabidhi mizinga ya nyuki kwa wazee wa koo zote kumi na mbili za Tarime Mjini na Vijijini, ikiwa ni hatua ya kuwaheshimu, kuwawezesha kiuchumi, na kutambua mchango wao mkubwa katika kulinda amani na utulivu wa jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meja Gowele alisema kuwa wazee ni nguzo kuu ya hekima, mshikamano na maadili katika jamii, hivyo ni wajibu wa serikali na jamii kwa ujumla kuendelea kuwathamini na kuwawezesha ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye maendeleo.
“Leo tunawakabidhi mizinga hii ya nyuki si tu kama njia ya kuwawezesha kiuchumi, bali kama alama ya heshima na shukrani kwa nafasi yenu muhimu katika jamii. Mmetufundisha kuwa amani huanza nyumbani, na nyinyi mmekuwa walinzi wakuu wa hilo,” alisema Meja Gowele.
Katika hatua ya kuonyesha mshikamano wa pamoja, Mkuu huyo wa Wilaya aliwashukuru kwa dhati wadau wote walioguswa na kutoa mchango wao kufanikisha zoezi hilo. Wadau hao ni pamoja na wanasiasa, wafanyabiashara, taasisi binafsi na mashirika ya kijamii.
Wadau waliotoa mchango mkubwa ni pamoja na:
1. Michael Kembaki
2. Dr. Edward Machage
3. Nyambari Nyangwine
4. Chichake
5. Eliakim Maswi
6. Esther Matiko
7. Simon Kiles
8. Daniel Komote
9. Neema Newland
10. Musa Ryoba
11. Hezbon Chacha Zablon (aka Machage)
12. Tiboche
13. God Kigoye
14. SOYA ONE LIMITED
15. Izack Range
Pia mchango mkubwa umetolewa na:
Halmashauri zote mbili (Mji na Vijijini)
Mashirika ya mazingira, usafi na maendeleo
Viongozi wa mila na ZTF – Tarime
Chama Cha Mapinduzi (CCM) – Wilaya ya Tarime
Kwa upande wao, wazee wa koo hizo waliokuwa wakipokea mizinga walionesha furaha na shukrani, wakimpongeza Meja Gowele kwa moyo wa kuthamini mchango wao. Aidha, walitoa pongezi maalum kwa kampuni ya Soya One Limited pamoja na wadau wote waliowakumbuka na kuwawezesha.
“Hatuna maneno ya kutosha kuelezea furaha yetu leo. Kukumbukwa na kiongozi wetu ni faraja kubwa, lakini pia kuona kampuni kama Soya One na wadau wengine wanajitokeza kutuunga mkono, ni jambo la kutia moyo. Tunawaombea kila la heri,” alisema mmoja wa wazee kwa niaba ya wenzake.
Tukio hilo limeibua matumaini mapya ya uhusiano bora kati ya serikali na wazee wa mila, likiwa ni mfano wa mshikamano unaojengwa kwa vitendo na kuhamasisha ushiriki wa kila kundi la kijamii katika maendeleo ya Tarime.



Comments
Post a Comment