Mdau wa Maendeleo Musa Ryoba Achangia Maji Katika Mkutano wa Wanawake na Vijana Wajasiriamali Tarime
Tarime, Mei 16, 2025 Mdau wa maendeleo na Mkurugenzi wa Mwanzo Mpya Foundation, Musa Ryoba, ameonesha moyo wa uzalendo na kujitoa kwa jamii kwa kuchangia katoni 20 za maji kwa ajili ya kufanikisha mkutano wa mwezi wa wanawake na vijana wajasiriamali wa Wilaya ya Tarime.
Mkutano huo muhimu umeandaliwa na taasisi ya Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) na kufanyika leo katika ukumbi wa BlueSky, ukiwaleta pamoja wanawake na vijana walioko kwenye sekta mbalimbali za ujasiriamali kwa lengo la kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujengewa uwezo wa kukuza biashara zao.
Katika mchango wake, Musa Ryoba alisisitiza umuhimu wa kuwainua wanawake na vijana kupitia fursa za kiuchumi na elimu ya ujasiriamali. “Nimeguswa na jitihada za TWCC katika kuwawezesha wanawake na vijana, ndiyo maana niliona ni vyema kuunga mkono mkutano huu. Maji ni kitu kidogo lakini muhimu sana katika mazingira ya mkutano,” alisema.
Mratibu wa mkutano huo kutoka TWCC alitoa shukrani kwa Musa Ryoba na kusema kuwa mchango huo umewezesha ufanisi wa shughuli zote zilizopangwa kwa siku hiyo. “Tunaamini ushirikiano wa wadau kama Musa Ryoba ni nguzo muhimu katika mafanikio ya shughuli zetu,” aliongeza.
Mkutano huu umekuwa jukwaa la majadiliano juu ya changamoto, mafanikio na fursa zinazowakabili wajasiriamali, huku pia ukitoa fursa ya mitandao ya kibiashara baina ya washiriki.


Comments
Post a Comment