TAASISI YA MARAFIKI WA MAENDELEO TARIME YAMWAGA VIFAA VYA TAALUMA VYENYE THAMANI YA MILIONI 40 KWA SHULE MBILI TARIME VIJIJINI
Kwa lengo la kuunga mkono juhudi za kuinua kiwango cha elimu katika Wilaya ya Tarime Vijijini, Taasisi ya Marafiki wa Maendeleo Tarime imekabidhi vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia vyenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 40 kwa shule mbili za sekondari — Magoto na Mbogi.
Kila shule imenufaika na kompyuta za mezani (desktop) mbili, kompyuta mpakato (laptop) moja kwa matumizi ya Mkuu wa Shule, na mashine moja ya kupiga nakala (photocopy machine) aina ya Canon. Vifaa hivyo vimepokelewa kwa furaha kubwa na walimu, wanafunzi na jamii inayozunguka shule hizo.
Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya taasisi, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Marafiki wa Maendeleo Tarime, Ndugu Martine Marwa, aliishukuru bodi ya taasisi hiyo pamoja na wadau mbalimbali waliotoa michango yao kwa moyo wa uzalendo.
“Tunaishukuru bodi ya taasisi yetu kwa kuratibu na kufanikisha upatikanaji wa vifaa hivi kupitia michango ya wadau wetu. Tunaamini kwamba uwekezaji katika elimu ni nguzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi,” alisema Marwa wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika shuleni Magoto.
Aidha, aliwataka walimu na viongozi wa shule kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vinatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa, hususan kusaidia maendeleo ya wanafunzi katika masomo ya TEHAMA na shughuli za kiutawala.
Kwa upande wao, walimu wakuu wa shule husika waliishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo mkubwa, huku wakisema kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi wa kazi na kuwapa wanafunzi fursa ya kujifunza kwa vitendo.
“Kompyuta hizi zitatusaidia sana katika kuandaa mitihani, kutunza kumbukumbu na kufundisha wanafunzi kwa njia ya kisasa. Tunaahidi kuvitumia kwa tija na kuvitunza ipasavyo,” alisema mmoja wa walimu wakuu.
Wananchi waliohudhuria hafla hiyo nao waliipongeza taasisi kwa moyo wa kizalendo, na kuiomba kuendelea kufanikisha miradi ya maendeleo katika sekta nyingine kama afya na maji.
Taasisi ya Marafiki wa Maendeleo Tarime imejizolea sifa kwa kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii kupitia misaada ya kielimu na kijamii, huku ikiwahimiza wadau zaidi kushirikiana kwa pamoja katika kuijenga Tarime mpya yenye matumaini na maendeleo endelevu.

Comments
Post a Comment