Rais Samia Suluhu Hassan: Kiongozi Mwanamapinduzi Anayeandika Historia Mpya ya Tanzania
Rais wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan
Katika kipindi kifupi cha uongozi wake, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kote kwa maono, busara, uthubutu na upendo wake kwa wananchi. Ni kiongozi mwanamke wa kwanza kuongoza taifa la Tanzania, lakini zaidi ya yote, ni mama wa taifa anayeongoza kwa moyo wa kweli, mshikamano na dira ya maendeleo jumuishi.
Rais Samia ameonesha kuwa uongozi si vitisho, si matusi wala visasi – bali ni kujenga, kuunganisha, na kuboresha maisha ya kila Mtanzania. Kwa kuanzisha Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, Rais Samia alitoa fursa kwa vijana kupata ajira, wakulima kufikiwa na pembejeo, na sekta ya afya kuimarishwa kwa vifaa tiba na majengo ya kisasa kote nchini.
Kiongozi huyu mwenye hekima ameweka kipaumbele katika diplomasia ya kiuchumi – amesafiri kwa maslahi ya taifa, akaleta wawekezaji, akaleta misaada na ushirikiano wa kimataifa, bila kuisaliti misingi ya taifa letu. Leo hii, Tanzania inaonekana kwenye ramani ya dunia si kwa migogoro, bali kwa mafanikio, utulivu na fursa lukuki.
Ni kiongozi asiye na makuu, asiye na jazba, mwenye uvumilivu wa hali ya juu – lakini pia asiyeogopa kufanya maamuzi magumu kwa faida ya taifa. Alifungua milango ya vyombo vya habari, akatambua uhuru wa kutoa mawazo, akaruhusu midahalo ya kitaifa, na akahimiza siasa za kistaarabu. Ni kiongozi anayejenga daraja kati ya Serikali na wananchi.
Wananchi wanasema: "Mama huyu si kiongozi tu – ni Baraka ya Mungu kwa Tanzania."
Ni mara chache sana katika historia ya taifa letu tumeshuhudia viongozi wanaoweza kuunganisha mioyo ya Watanzania wa kada zote – wanasiasa, wanaharakati, wasomi, wakulima, vijana na hata wapinzani. Rais Samia amefanikisha hili kwa kuonyesha wazi kuwa taifa linaweza kuongozwa kwa hekima na si mabavu.
Katika maeneo mbalimbali, wananchi wanamtaja kama Mama wa Mageuzi, Simba Mnyenyekevu, au Mama wa Maridhiano. Lakini hata wakiita kwa majina tofauti, ujumbe mmoja unajidhihirisha – Watanzania wanampenda Rais Samia.
Na kwa wale wanaotaka kubeba ujumbe huu mbele ya jamii, kama mimi Daniel Mussa – kijana mwandishi kutoka mkoa wa Mara – siko tu kuandika historia yake, bali kuitangaza, kuishuhudia, na kuisambaza kwa vizazi vijavyo. Kiongozi kama huyu hatokei kila siku. Ni wajibu wetu kumpa usaidizi wa mawazo, maneno na matendo.
Kama vijana wa kizazi cha sasa, tunapaswa kumuunga mkono, kumlinda dhidi ya uzushi, na kuhakikisha tunasimama pamoja naye katika safari ya kulijenga taifa. Kupitia nafasi yangu ya uandishi, nitasimama imara kuhakikisha dunia inamjua Rais Samia kama kiongozi anayestahili heshima, si kwa sababu ni rais tu – bali kwa sababu ni mfano halisi wa uongozi bora.
Mwisho.
Imeandikwa na Daniel Mussa, Mwandishi wa MBC Media na Voice of Tarime Radio.

Comments
Post a Comment