TATHMINI YA HALI YA KISIASA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025, KWA CHAMA CHA MAPINDUZI.
04.04.2025
Ndugu wananchi wenzangu na wanachama wenzangu wa chama cha mapinduzi pamoja na wadau mbalimbali kutoka Tarime mjini kwa unyenyekevu mkubwa sana nawasalimu wote.
Napenda kuwajulisha kuwa nilipokea maoni kutoka kwa watu mbalimbali wakiomba tathmini ya hali ya kisiasa ya jimbo Tarime mjini kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025 uchaguzi utaoanzia ndani ya Chama cha Mapinduzi ili kupata mwakilishi makini na atayekubalika atakaye pewa ridhaa ya kuwakilisha chama katika hicho katika uchaguzi mkuu ujao mapema October 2025
Tathmini hii ni imebeba sehemu kubwa ya maoni wanachama, wananchi wa jimbo la Tarime mjini na wadau wa siasa ndani na nje ya Tarime mjini. Hii inaweza kutumika kama msingi wa kutaka kufahamu ukweli zaidi kwa anayehitajika lakini ndivyo hali ya siasa ilivyo kwa sasa tarime mjini.
Kabla ya kuanza naomba nianze na utangulizi huu kama *reference* na shuhuda za wazi huko duniani.
*Wakati Yuda ikiongozwa na kiongozi mzuri na mwenye haki kama Yosia, taifa lilistawi. Lakini ilipokuwa chini ya mwovu Manase, taifa lilisambaratika. Katika karne hii, Uingereza ilipata msukosuko mkubwa mwaka 1936 juu ya uamuzi wa Edward VIII kuoa mwanamke wa Kimarekani aliyekuwa mtalaka Wallis Simpson*
Hivyo basi ni wajibu wa wanatarime kujua ni kiongozi wa aina gani anahitajika kwa wakati huu kwa mstakabali wa maendeleo ya wanatarime mjini na hili halihitaji kufanyiwa majaribio hata kidogo bali tafiti za kisayansi.
Hivyo basi kwa vyovyote vile ni muhimu sana wananchi wa Tarime mjini kuhakikisha kuwa wanaowajibu wa kuhakikisha kuwa jimbo la Tarime mjini linapata kiongozi sahihi ambaye atakuwa kama joshua mwenye maono ya kweli na atayekubalika kwenye makundi yote na siyo kiongozi anayegawa watu kwa itikadi za vyama kiongozi mwema weledi na kiu ya kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi wa Tarime mjini.
A. *NAOMBA KUTOA HISTORIA FUPI YA JIMBO LA TARIME MJINI.*
1. Jimbo la Tarime mjini lilianzishwa rasmi mwaka 2015 baada ya mgawanyo jimbo la Tarime na kupata majimbo mawili. Yaani Tarime mjini na Tarime vijijini. Ni jimbo ambalo kama lilivyo jimbo la Tarime vijijini linakaliwa na watu wa jamii ya Wakurya kama wazawa wa jimbo, japo yapo makabila mengine ambayo pia ni wakazi wa Tarime mjini japo kwa asilimia ndogo sana.
2. Utamaduni wa watu wa Tarime una historia yake na msisimko mkubwa kwa sababu siyo watu waoga ni watu wakweli na wachapa kazi na bila kupepesha macho wala kumung'unya maneno. Ni watu wanaoshi kwa kuzingatia miiko mila na desturi pamoja na historia ya urithi wa tunu za wazee wao kutoka enzi na enzi.
3. Ukweli uliowazi ni kwamba jimbo la Tarime mjini kwa jinsi lilivyo, liligawanywa kisiasa zaidi kuliko ilivyokuwa uhalisia au ilivyofikiriwa au kukusudiwa hapo awali. Chanzo cha kuipa Tarime mjini eneo dogo lilikuwa ni hisia za kisiasa kwamba mwaka 2015 John Heche angegombea Tarime mjini, eneo ambalo alishawahi kuwa diwani wake, wakati huo ikiitwa kata ya Tarime mjini. Lengo na mafikirio ilikuwa kwamba Heche kutokea Chadema endapo atashinda Tarime mjini, basi kijijini atashinda *Mzee Christopher Kangoye* wa CCM na hivyo Tarime vijijini watakuwa na vyanzo vingi vya mapato.
4. Kitu kilichoishangaza CCM ni kwamba Heche aligombea vijijini na *Ester* *Matiko* ambaye hakuwa anafikiriwa kama angekuwa na ushawishi kwenye jamii hii ya kurya kutokana na mila na desturi aligombea mjini na akashinda kwa kushindo na kulichukua jimbo la Tarime mjini Ikumbukwe kwamba ilikuwa ni mara ya kwanza jimbo la watu wa jamii ya Wakurya popote pale kuongozwa na mbunge wa kike kupitia sanduku la kura kwenye uchaguzi mkuu. Lakini katikati ya mila, na desturi na tamaduni za Kikurya zilizomnyima mwanamke fursa ya kuongoza tangia zamani huku mila hizo zikiamini kuwa mwanamke ni mtu wa kuolewa tu na siyo kuwa kiongozi kwenye jamii hii lakini ikawa kinyume chake na mwiko huu ukavunjwa na binti wa Kikurya Ester matiko na akaibuka kuwa shujaa katikati ya miamba ya kiume na kuvunja vikwazo vyote vya mila za Kikurya mwisho wa siku Esta Matiko akawa shujaa na kuibuka kuwa mbunge wa jimbo la Tarime mjini hadi mwaka 2020.
5. Bila kusahau Historia zinaonyesha kuwa Esta Matiko alichangia kwa kiasi kikubwa usindi wa john heche kwenye maeneo ya koo anazotokea huko bumera,bunchari na maeneo yote ya jamii ya kurya kwenye uchaguzi wa 2015.
6. Wakati tunaingia kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, Esta Matiko alirudi tena kutetea nafasi yake; lakini kutokana na mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo wakati huo sote tunajua kilichotokea kimsingi hakuweza kushinda uchaguzi kwa lugha nyepesi hakutangazwa japo kungekuwa na uwazi hadi leo ndiye angekuwa mbunge wa tarime mjini Hivyo kwa mtaji huo Mhe. Michael Kembaki akaokota embe dodo chini ya mwembe na akawa ametangazwa kuwa mbunge wa tarime mjini japo kwa ushindi kiduchu.
B. *NANI ANAFIKIRIWA KUWA NA USHAWISHI MKUBWA KWENYE UCHAGUZI WA 2025 TARIME MJINI?*
1. Kwenye hekaheka za kisiasa jimbo la Tarime mjini hasa kupitia CCM yapo majina ambayo yanatajwa sana Majina haya yanatajwa kwa wanachama, wajumbe,wananchi wa Tarime mjini pamoja na watumiaji wa mitandao ya kijamii WhatsApp group n.k na Watu hawa ni pamoja na Ester Matiko, Chonchorio, Jackson Kangoye, Michael Kembaki na Said Chambiri. Joyce Mago ambaye ni MNEC yeye ameamua kuchukua njia ya viti maalumu.
2. Hoja hapa ni nani Sasa mwenye ushawishi na nguvu ya kushinda uchaguzi katika kura za maoni ndani ya ccm pamoja na uchaguzi mkuu ujao utaohusisha vyama vyote?
MAONI YANGU NA MAONI YA WANANCHI WA TARIME MJINI.
2.1 *ESTER MATIKO*
Huyu bado anahesabika kwamba ni mbunge wa viti maalumu kupitia chadema. Lakini kutokana na mzozo waliokutana nao kwenye chama chao, anatambua wazi kuwa siyo mwanachama pamoja na wenzake 18 kutokana na chama chao kuwafuta uanachama. Wabunge hawa walikuwa na matumaini makubwa kwamba endapo Mhe. Freeman Mbowe angeshinda nafasi ya Uenyekiti wa chama chao angeweza kuwarudisha kwenye chama. Lakini ushindi wa Lissu na Heche unaonekana kuwa kikwazo na mwiba kwao kurejea. Hii ni kutokana na msimamo wao, na wasiwasi wao mkubwa ni kwamba hata kama watarudi wanaweza wasipewa nafasi ya kugombea kwenye uchaguzi unaokuja hata kama wana nguvu kiasi gani. Hivyo chaguo pekee walilonalo iwe jua au mvua au kwa vyovyote vile ni kuhama chama chao cha zamani ambacho kimsingi hakiwatambui hadi sasa
2.1.1 Ikizingatiwa kuwa sehemu kubwa ya watu waliokuwa na Mhe. Easter Matiko wakati alipokuwa anahangaishana na chama chake wamesharudi CCM na wengine pia ni wenyeviti wa serikali za mitaa akiwemo sabato amos pamoja na okendo na wengine ni wajumbe kupitia CCM. Hivyo, hatuna shaka kwamba kama Mhe. Matiko ataamua kuondoka Chadema bila shaka ataenda CCM. Hivyo watu wake waliotangulia tunaweza kusema walienda kuandaa mazingira ili wakati ukifika basi awe na watu wa kumpokea ccm ukilinganisha kuwa siku za hivi karibuni amekuwa na ukaribu fulani na wadau wa chama cha mapinduzi.
*Mwenekano wa ESTA MATIKO kwa sasa na ushawishi wake ukoje kwa siasa za Tarime mjini?*
2.1.2 Esta Matiko anazifahamu siasa za Tarime. Ni mtu ambaye ameweza kuvuka miiko na vizingiti na vikwazo vingi vya kitamaduni kwamba mkurya hawezi kuongozwa na Mwanamke. Lakini pia ni mtu ambaye tayari amejiandaa kiakili na kisaikolojia kwamba hahitajiki tena Chadema. Na hivyo kwa vyovyote vile anatamani kuendelea kufanya siasa kupitia CCM ili aendelee kutimiza mipango yake ya kuleta mageuzi kwenye jamii hii ya kurya ili kuondoa dhana kuwa wanawake hawawezi kushika madaraka .
Esta ni mtu ambaye anauwezo binafsi na analimudu jukwaa la siasa ziwe za joto au baridi ziwe za upinzani au ndani ya ccm kutokana na mtaji mkubwa alionao wa kukubalika kwenye jamii na hasa tarime mjini.
Esta Anao uwezo wa kujenga hoja na kufanya ushawishi na amezoea siasa za mchakamchaka. Alipokuwa bungeni pamoja na kwamba siyo mbunge wa jimbo, amekuwa sauti ya watu wa mkoa wa Mara na Tarime yake bila kujali mlengo wa chama chake bali dhana ya maendeleo kwa jamii yake ya mara.
Esta siku zote hajawahi kupungukiwa wala kupwaya.
JE *ESTA MATIKO anaweza kuaminiwa na CCM Tarime Mjini?*
2.1.3 Swali la msingi ni nafasi yake ya kuaminiwa. Kama aliweza kuaminiwa 2015 jimbo likiwa jipya na akashinda tena kwa kura nyingi, na 2020 kuna uwezekano mkubwa kwamba hakutangazwa kutokana na aina ya siasa zilizokuwepo, bila shaka ni mtu mwenye ushawishi ambaye anaweza kufanya balance nzuri kwenye upinzani kwa kuwa anazijua siasa zote
Na hasa ukiangalia ushawishi wake kwa makundi mbalimbali ya wana Tarime mjini bila kujali itikadi ya vyama, bila shaka anaweza kuwa mtu sahihi kama atajiunga na CCM na kupewa fursa ya kugombea. Nasema hivyo kwa sababu, Kwanza, anaomtaji wa watu waliomuunga mkono tangu 2015. Pili anaweza heka heka za siasa za majukwaani na field. Tatu, ataipunguzia nguvu chadema na kuidhoofisha kabisa kutokana na ushawishi wake ikizingatiwa kwamba kwa sasa hawana mtu ambaye ni icon tofauti na watu kama Bob Wangwe na Sauti ambaye ushawishi wao hauwezi kuulinganisha na Esta. Nne, ni mtu ambaye pamoja na kwamba ni Mwanamke hahitaji kubebwa kwa ajenda za ujinsia akisimama jukwaa anakuwa ameenea pande zote.
Na kama kweli tunataka kufanya mambo ya gender balance basi, Esta anaweza kuwa ni mtu sahihi kwa sababu itahitajika support kidogo kwake.
2.1.4 Pengine jambo ambalo wengi hawatilii maanani sana, japo ni lazima lisemwe ni kwamba kabla ya kuvuliwa uanachama wake alikuwa ni Mwenyekiti wa kanda ya Serengeti. Alipata nafasi hiyo baada ya kumshinda John Heche ambaye sasa hivi ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema taifa, Bara. Kwamba pamoja na kwamba Heche anajulikana kwamba ni wa moto lakini alishindwa uchaguzi na Ester Nicolaus Matiko. Huyu ni mtu ambaye CCM inapaswa kumwangalia kama fursa ili kuliweka jimbo la Tarime mjini katika hali isiyo na mashaka ya kunyakuliwa na upinzani. Kwa nyakati zote, chama cha siasa kinalenga kushika dola na kuongoza serikali. Siyo aibu chama kutumia ushawishi wake kumvuta Esta Matiko ndani ya chama ili aongeze nguvu kwenye mapambano ya kumsaidia Mhe. Rais kutafuta kura, lakini pia kuleta maendeleo. Uzoefu wake kama mbunge kwa miaka 15, na mbunge wa umoja wa mabunge duniani inampa fursa na uzoefu mzuri. Na hivyo anakuwa ni fursa ya kuendelea kutumiwa kwa maslahi mapana ya chama na taifa.
2.1.5 Kawaida wanasiasa na watu ambao wamebaki na legacy zao hapa duniani hupenda kujitofautisha na wengine kwa jinsi ya kuwaza na kufanya mambo yao. Na kawaida hupenda kuacha alama ambazo haziwezi kufutika kwenye maeneo yao kwa vizazi vingi vijavyo. Esta Matiko amejaribu kusemea mambo na yatafanyika. Haya ni mambo ambayo hata leo Esta akitoka kwenye siasa daima itabaki kuwa kwenye kumbukumbu za jamii kwamba bila yeye pengine visingeweza kufanyika, au vingechukua muda mrefu kufanyika au visingefanyika kwa namna ambavyo vimefanyika. Na yawezekana hata sasa Esta akiulizwa mambo matano makubwa na ya kihistoria aliyoyapigania wakati wa ubunge wake, basi hawezi kukosa kutaja yafuatayo. Moja, Esta Matiko amekuwa sauti kuu ya wananchi wa Kenyambi na Bugosi kulipwa fidia kupisha JWTZ. Pili, sauti yake juu ya ujenzi mnada wa Magena haiwezi kusahaulika kamwe. Tatu, ni Esta ndiye aliyeshika shilingi ya waziri bungeni hadi serikali ikatenga bajeti ya soko la Remagwe. Mnaweza kukumbuka kwamba wakati wa ziara ya waziri mkuu, Mhe Waitara alisema kuwa soko hilo litajengwa na fedha za ndnai bila hata kujua ukweli wa chanzo cha fedha hizo. Nne, soko kuu la Tarime ni mradi ambao Esta Matiko aliomba kipindi akiwa mbunge wa jimbo. Tano, Ujenzi wa miundombinu kama barabara ya Lami kuunganisha majimbo ya Tarime mjini, Tarime vijijini na Serengeti, pamoja na dampo na stendi ya Kemange ni sehemu ya miradi ambayo mchango wa Esta Matiko siyo wa kutiliwa shaka. Kama ilivyo kazi ya mbunge kwamba ni kutunga sheria, kushauri na kuisimamia serikali, na kuwakilisha wananchi bungeni, basi Esta Matiko ameifanya kazi hiyo kwa weledi, moyo na juhudi zote. *Hivyo, ESTA MATIKO ANAPEWA 55% ZA USHINDI KAMA CHAMA CHA MAPINDUZI IKIWA KITAWEZA KUMCHUKUA NA KUMSIMAMISHA KUWA MGOMBEA JIMBO LA TARIME MJINI NA HAYA NI MAONI YA WANANCHI WA TARIME MJINI.*
2.2 CHONCHORIO NI NANI NA YUPO KATIKA NAFASI GANI KISIASA.
Huyu ni mjumbe wa mkutano mkuu wa taifa. Ni kijana wa Tarime, aliyezaliwa na kukulia kwa kiasi kijiji cha Borega. Ni mfanyabiashara ambaye kwa miaka ya hivi karibuni amejiwekeza kwenye siasa. Ni mtu ambaye kundi la vijana ni sehemu kubwa ya wafuasi wanaomuunga mkono. Pamoja na ukweli kwamba anatumia rasilimali fedha kubwa kujinadi na kujitangaza kwenye jamii na kijana mkarimu sana lakini hisia za kwamba siyo Mtanzania zinaweza kutia dosari safari yake ya kisiasa hilo ni kutokana na historia ya hivi karibuni ilijitokeza na kuripotiwa na vyombo vingi vya habari pamoja na mitandao ya kijamii.
2.2.1 Hisia hizi zilichagizwa zaidi ni kauli za mbunge wa Kenya ambaye Bw. Chonchorio alimwalika kwenye shughuli yake Tarime na kuanza kukinanga chama cha Mapinduzi na serikali ya JMT. Mbunge yule kwa wanaomfahamu wanasema ni ndugu wa damu wa Chonchorio na hivyo kuweka mashaka makubwa juu ya uraia wa Chonchorio na mahusiano na mbunge wa Kenya.
2.2.2 Kitu pekee ambacho Chonchorio amejaliwa ni moyo ya kujaribu pamoja na ukarimu tukumbuke kuwa alijaribu kwenye ujumbe wa mkutano mkuu wa taifa na ameshinda, amejaribu biashara na kufanikiwa. Lakini kwenye siasa za Tarime mjini, jina lake kwa kadri siku zinavyoenda linazidi kupotea. Pengine ni kwa sababu hakuwekeza vya kutoka kwa watu ambao wanaweza kumpa ushauri na mikakati ya namna ya kudumu kwenye mapambano ya kisiasa. Sehemu kubwa ya vijana alionao na wanaomuunga mkono ni wa kusifia na kupamba kwa jina maarufu la chawa. Sehemu kubwa ya kundi hilo kwa sasa wameishamia kwa watia nia wengine ambao wameonekana kuwa na mipango endelevu. Ndiyo maana kwa sasa ni nadra kukuta jina la Chonchorio likitajwa tajwa kwenye magroup tofauti na ilivyokuwa awali na hata kurusha picha zake kwa nia ya kumtangaza mpango ambao umefifia na kwenye analysis yangu unanipa nafasi ya kutoa maoni yangu.
2.2.3 Ninachelea kusema, hadi tunafika mwezi Julai kwenye mchakato wenyewe jina lake litakuwa halisikiki kabisa. Sababu kubwa ni kwamba aliwekeza zaidi kwa chawa ambao muda wowote wananunuliwa na kuuzika kama bidhaa zingine sokoni Pamoja na hilo, sioni nafasi yake ya ushindi wa ubunge hata kama atatumia fedha kiasi gani kushinda kura za maoni. Hii ni kwa sababu, siasa za Tarime kwa ujumla kwa miaka ya hivi karibuni ni siasa za heka heka sana zinazohitaji akili kubwa na maarifa ya kutosha Mashaka ni makubwa kama ataweza kukabiliana na nguvu ya upinzani ikizingatiwa kwamba Mhe. Heche ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema naye atakuwa anaongezea nguvu Tarime mjini akitokea Tarime vijijini. Na kwa sababu Bob Wangwe na Heche ni marafiki tayari, na pia Heche alishasema alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara Nyamongo kwamba akisimama vijijini Bob atasimama mjini ni wazi kabisa atamwongezea Bob nguvu hivyo eneo hilo linahitaji ukuta imara sana ambao siyo rahisi kubomolewa kwa gharama nafuu.
2.2.4 Sasa kama hiyo nguvu itaongezeka kwa Bob ni wazi kabisa anahitajika mtu mwenye misuli ya kupambana na nguvu hiyo. Chonchorio hana uzoefu wa siasa za majukwaani, na pia uwezo wake kwenye jukwaa na ushawishi kwa watu siyo wa kiwango cha juu. Hivyo kuna uwezekano mkubwa akagalalazwa mchana kweupe nanmgombea wa upinzani kama atasimamishwa yeye kugombea kwa upande wa CCM.
HIVYO BASI KWA HALI ILIVYO KWENYE GROUND, BWANA CHONCHORIO ANAKUWA NA 08% ZA USHINDI TARIME MJINI
2.3 *MICHAEL KEMBAKI.*
Huyu ni mbunge wa sasa wa jimbo la Tarime mjini. Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge mwaka 2020. Ni mtu ambaye ashindwa vibaya kwenye kura za maoni ndani ya chama mwaka 2020 na akashika nafasi ya tatu tena kwa tofauti kubwa sana ya kura. Lakini aliwashangaza wengi baada ya chama kurudisha jina lake ili akipeperushe chama cha Mapinduzi. Ni mtu ambaye amekuwa mbunge, lakini sauti yake bungeni kuhusiana na Tarime imekuwa hafifu sana kwa muda wote.
2.3.1 Kembaki kwa sehemu kubwa siyo mtu wa kujibizana na watu kwenye mitandao ya kijamii kama alivyo mbunge wa tarime vijijini ambaye anashinda mitandaoni kujibizana ns wapiga kura wake Kembaki Ni mtu wa vitendo zaidi. Akisemwa kwenye mitandao anaona na kufanyia kazi masuala yanayolalamikiwa. Kwa sehemu ametatua changamoto za watu wa Tarime mjini. Japo bado kuna changamoto ya barabara mjini kwa sababu barabara nyingi ni za vumbi. Stend nzuri inayoakisi hali ya mji wa Tarime haipo na yeye na Halmashauri yake wameshindwa kubuni vyanzo vipya vingine vya mapato. Soko la kisasa la Tarime mjini linaweza kumwongezea alama japo ni Esta Matiko ndiye shujaa anayesikika sana bungeni akilizungumzia pamoja na hospitali ya wilaya ya Tarime hatujawahi kumsikia Kembaki akiuliza hata swali la nyongeza bungeni kuhusu soko au mipango mingine ya maendeleo ya Tarime zaidi ya miradi ya mama Samia Suluhu Hassan.
2.3.2 Changamoto kubwa ya Kembaki ni uwezo wake wa kushawishi maana siyo mzungumzaji. Hana timu nzuri ya kumzungumzia wala kuzungumza mambo aliyoyafanya au kufanywa na serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Ni mtu ambaye akigundua kuna mtu anampango wa kutia nia ni kuanza kumtafuta na kuanza fitina. Mfano, ni tuhuma za kuandaa vijana ili wamzomee Esta Matiko mbele ya Waziri Mkuu kwenye uwanja wa Shamba la bibi alipofanya ziara ya mwisho Tarime huu ni ushahidi tosha wa fitina zake .
Anstegemea kukutana na ukinzani mkubwa ndani ya chama (wajumbe) kwa sababu wanaamini kwamba hakuwa chaguo lao kutokana na kushindwa kwake kwenye kura za maoni hilo asije akasahau kuna wajumbe wanamsubiri hadi kesho ..
Kembaki ni mtu ambaye amefanya makosa ya kiufundi kwa kuungana na mbunge wa Tarime vijijini (Waitara) kuleta mafarakano na fujo kwenye chama na pengine muunganiko huo unaweza kumpotezea nguvu na kukosa kura ndani ya chama cha mapinduzi Pamaja na hayo, changamoto kubwa iliyo mbele yake ni uwezo wake wa kukabiliana siasa za upinzani ndani ya jimbo hilo nalo ni kubwa mno.
Kama ilivyoainishwa kwamba hana uwezo wa kumiliki jukwaa, hivyo kuna hatari ya kulipoteza jimbo kwa asilimia 85 % kama dola haitatumia mkono wake.
2.3.3 Mhe. Kembaki ambaye amekuwa mbunge kwa miaka mitano sasa, amekosa ubunifu wa kuanzisha au kupendekeza uanzishwaji wa miradi ya kimkakati ndani ya jimbo na Halmashauri yake. Huduma za jamii kama shule, barabara, afya ni huduma za msingi ambazo serikali inatekeleza kwa sababu ziko kwenye ilani. Lakini miradi ya kimkakati huwa inalenga kukupanua wigo wa wananchi kufanya biashara, kupanua masoko ya bidhaa za wananchi na kuongeza mapato ya Halmashauri. Katika eneo hili, Mhe. Kembaki amekosa ubunifu kabisa kwa sababu hajaweza kufikiria na kubuni jambo kama hilo kama ambavyo ameweza kufanya mwenzake Esta Matiko. HIVYO BASI KWA UFAFANUZI HUO, KEMBAKI ANAWEZA KUWA NA 25% ZA USHINDI KATIKA JIMBO LA TARIME MJINI.
NB: ASILIMIA 12 ZINAZOBAKI WATAGAWANA WALIOBAKI NA WENGINE AMBAO WANAWEZA KUJITOKEZA.
Ninapenda kuhitimisha kwa kushauri kwamba, ni vyema sana chama cha Mapinduzi kikaangalia watu ambao watakivusha chama kwenye uchaguzi mkuu bila kuhitajika kutumia nguvu za ziada. Ukweli ulio bayana ni kwamba ushindi wa mwaka 2020 siyo kigezo kizuri cha kupima hali ya kukubalika kwa waliotangazwa kwa sababu ya mazingira ya kisiasa yaliyokuwepo. Ni rahisi hata sasa mgombea kutumia rushwa kushinda kura za maoni, na tukadhani ni ameshinda kwa sababu ya hali ya kukubalika kwake kumbe chama kikumbana na upinzani mkubwa kwenye uchaguzi mkuu.
Mungu awabariki sana, Kila la kheri katika kuwapata wawakilishi wenye manufaa na wa kuifaa jamii yetu.

Comments
Post a Comment