MBUNGE VITI MAALUM GHATI CHOMETE NA MBARAZA MARIAM SAGINI WAAHIDI KUONGEZA WANAFUNZI CHUO CHA LAKE VICTORIA DISABILITY VOCATIONAL TRAINING CENTRE
Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Mara Mhe. Ghati Chomete ameahidi kushirikiana na Mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa Ndg. Mariam Sagini kuhamasisha na kukitangaza Chuo cha Lake Victoria Disability Vocational Training Centre ili wanafunzi waongezeke kutokana na uwezo wake wa kubeba wanafunzi zaidi 600 ila mpaka sasa kina wanafunzi 65.
Akizungumza wakati alipomwakilisha Mgeni Rasmi Mjumbe wa Baraza Kuu UWT Taifa Ndg. Mariam Sagini katika mahafali ya nane yaliyofanyika chuoni hapo Novemba 22, 2024 katika Kijiji cha Nyabange, Kata ya Nyankanga, Wilaya ya Butiama Mhe. Chomete amesema chuo hicho kina mchango mkubwa katika kuwapa vijana wenye ulemavu na wasio na ulemavu fursa ya kujifunza na kujiendeleza.
"Habari njema ni kwamba chuo hiki pamoja na kutoa huduma ya elimu ya ufundi nimeambiwa mnatoa huduma ya utengamao kwa watu wenye ulemavu kama mazoezi tiba, kazi tiba, utengenezaji wa viungo bandia, vifaa saidizi kama baiskeli za watu wenye ulemavu, magongo ya kutembelea, viti vya kona nk. Hii inapaswa jamii ione kama fursa katika ulimwengu wa sasa walete vijana wajifunze hata pia lugha ya alama," amesema Mhe. Ghati.Pia Mhe. Chomete amewaasa wahitimu kuwa wajitangaze kwa chuo walichotoka cha Lake Victoria Disability Vocational Training Centre na taaluma walioipata ili iwe rahisi kupata kazi na kutengeneza kipato chao wenyewe kuliko kukaa nyumbani kwani itakuwa kero kwa wazazi na mwisho watawaona kama mizigo ukizingatia walitumia pesa nyingi kwa ajili ya kuwasomesha.
Pia Kaimu Mkurugenzi wa Chuo cha Lake Victoria Disability Vocational Training Centre amesema chuo hicho kilianza mwaka 2002 na kimesajiliwa chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Elimu Stadi (VETA) kwa ngazi ya cheti daraja la pili hadi sasa kinatoa kozi fupi na ndefu za Uselemala, uchomeleaji vyuma, ushonaji mapambo, ufundi bomba, ufundi umeme, TEHAMA, ufundi viyoyozi na majokofu, madini, usaidizi wa maabara, utalii, uhazili, mapokezi, utunzaji nyumba na mapishi ambapo Jumla wahitimu 30 wamehitimu katika fani mbalimbali.
Aidha Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Lake Victoria Disability Vocational Training Centre Egata Magafu ameeleza kuwa chuo hiko kwa kushirikiana na taasisi ya Tanzania Club Foot Organisation kinatoa na huduma ya matibabu ya miguu kifundo bure kwa watoto waluo chini ya umri wa miaka mitano, ambapo matibabu hufanyika kuanzia hatua ya awali hadi hatua ya mwisho kuhakikisha miguu ya watoto hao inarekebishika kikamilifu.









Comments
Post a Comment