MHE ESTHER MATIKO KUTOA MILIONI ISHIRINI TARIME SEKONDARI (20,000,000/=)
Mhe Esther Nicholas Matiko Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara ambaye ni Mkurugenzi wa taasisi ya Matiko Foundation ameendelea na ziara yake ya kibunge ndani ya Mkoa wa Mara.
Akiwa Shule ya Sekondari Tarime inayopatikana Tarime Mjini, Mhe Mbunge amefika shuleni hapo na kuzungumza na Walimu pamoja na Wanafunzi wa Shule hiyo ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kufanikisha upatikanaji wa matokeo mazuri ya kidato cha sita.
Mhe Esther Matiko akizungumza na Wanafunzi hao, ameahidi kutoa kiasi cha Shilingi Milioni Ishirini (20,000,000/=) kupitia taasisi ya *_Matiko Foundation_* iwapo Shule hiyo itafanikiwa kupata matokeo ya Daraja la kwanza (Division One) kwa Wanafunzi wote wa kidato cha sita wanaotarajiwa kufanya mitihani yao mwakani 2025.
Mhe Mbunge ametoa ahadi hiyo ikiwa ni jitihada za kuunga juhudi za Serikali chini ya Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Kampeni yake ya kutoa Ufadhili wa kwa masomo ya Sayansi *(Samia Scholarship)* kwa wanafunzi wanaofaulu daraja la kwanza kwa alama tatu (Div 1 Point 3).
Kupitia Samia Scholarship, Shule ya Tarime Sekondari imefanikiwa kutoa wanafunzi watatu waliofikia vigezo vinavyohitajika. Kampeni hiyo imeanzishwa shuleni hapo kupitia mashindano ya michezo mbalimbali ikiwa na kauli Mbiu isemayo “Mama Kwanza, Division One ya Point Tatu Inawezekana”.
Mhe Esther Matiko ameunga mkono kampeni hiyo shuleni hapo kwa kutoa vifaa vya michezo mbali mbali kwa ajili ya mashindano ambavyo ni Jezi seti moja ya mpira wa Miguu, Mipira miwili ya Kikapu (Basketball), Mipira miwili ya miguu(Football), Mipira miwili ya Wavu (Volleyball) Mipira miwili ya mkono (Handball), goalball mmoja na Mbuzi mmoja, vyote vikiwa na thamani ya Tsh milioni moja na laki nne (1,400,000/=)
Ikumbukwe, Mhe Esther Matiko alitoa ahadi ya Tsh 10,000,000/= mwaka 2023 kwa Shule hiyo iwapo wangefanikiwa kupata daraja la kwanza na pili pekee kwa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu (2024), licha ya kwamba Shule hiyo haikufanikiwa kufikia lengo, Mhe Esther Matiko ametoa kiasi cha Tsh 500,000/= kwa ajili ya Lunch kwa Walimu wa Shule hiyo ikiwa ni motisha kwa kuiwezesha Shule hiyo kuongoza Tanzania nzima kwa kuwa na Division One nyingi zipatazo 355.
Mhe Esther Matiko amesema ni matamanio yake kuona siku moja Tarime Sekondari ikipewa hadhi ya Shule Maalum (Special School) kutokana na matokeo mazuri ya kitaaluma itakayoyapata kupitia kwa Wanafunzi, Walimu, Wazazi na Wadau wengine wa elimu.
Mkuu wa Shule hiyo Mwl Chenge hakusita kutoa pongezi na Shukrani za Shule hiyo kwa Mhe Esther Matiko kwa jinsi anavyoshirikiana na shule hiyo kwa kutatua changamoto mbali mbali na hivyo kusaidia kuinua viwango vya taaluma shuleni hapo.
Itakumbukwa Mhe Esther Matiko alipata kuwapeleka bungeni Walimu na Watumishi wa Tarime Sekondari kwa matokeo mazuri ya kidato cha sita 2023, Walimu wa Shule hiyo waliweza kupata fursa ya kukutana na viongozi mbali wa kiserikali na kuwasilisha hoja zao akiwemo…
Mhe Dotto Biteko (Naibu Waziri Mkuu), Mhe George Simbachawene (Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Mhe Kipanga Naibu Waziri Elimu na kuwawezesha kushiriki maadhimisho makubwa ya siku ya Walimu wilayani Bukombe kwa mwaliko maalum wa Mhe Dotto Biteko Naibu Waziri Mkuu.



Comments
Post a Comment